NASABU YA SAYYIDINA ABUBAKAR
Jina lake ni Abdullah bin Othman bin Amer bin Amru bin
Kaab bin Saad bin Tayim bin Murrah bin Kaab bi Luay Al Kurashiy Al Taymiy, na
uhusiano wake na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) unakutana kwa Murrah
bin Kaab, kwani jina la Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Muhammad
bin Abdillah bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdu Manaf bin Qusay bin Kilab bin Murrah bin Kaab.
Jina la baba yake ni Othman, lakini alikuwa maarufu kwa
jina la Abu Quhafah, kwa hivyo Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa
akijulikana kwa jina Ibni Abi Quhafah, yaani mwana wa Abu Quhafah.
Mama yake ni Ummu l Khayr – Salma binti Sakhar bin Amer
bin Kaab bin Saad bin Tayim bin Murrah bin Kaab na alikuwa binti ammi
yake Abu Quhafah.
WAKE ZAKE NA WANAWE
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alioa wake wanne;
Wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu) alimuoa Qutailah
binti Saad na akazaa naye Abdullah na Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Abdullahi aliingia katika Uislamu tokea siku za mwanzo
na alifariki wakati wa ukhalifa wa baba yake.
Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni maarufu kwa jina la
'Dhaat nitwaqayn', na alipewa jina hilo baada ya kukata 'Nitaaq' mkanda wa
kitambaa kinachofungiwa nguo kiunoni na kukifunika chombo kilichotiwa chakula alichokuwa
akipelekewa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhajir kwenda Madina, na alikuwa
mkubwa kwa umri kuliko Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha).
Aliolewa na Al Zubeir (Radhiya Llaahu ‘anhu) walipokuwa
Makkah na alizaa naye watoto wengi mpaka alipomuacha akawa anaishi kwa mwanawe
Abdullah bin Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyeuliwa Makkah.
Bibi Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anha) aliishi miaka mia, na
mwisho wa maisha yake alikuwa kipofu.
Wakati wa ujahilia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alimuoa pia Umm Rumaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyezaa naye Abdul
Rahman na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) mke wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) na alifariki dunia wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) aliyeteremka kaburini kwake siku ya maziko na kumuombea maghfira.
Abdul Rahman alipigana vita vya Badr na vita vya Uhud
akiwa upande wa makafiri, na kabla ya kuanza vita vya Badr aliita kwa sauti
kubwa akitaka mtu yeyote upande wa Waislamu aje kupambana naye na Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alipotaka kutoka na kupambana na mwanawe huyo, Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimzuwia na kumwambia;
"Tuache tukufaidi.".
Abdul Rahman alikuwa shujaa na mtupa mshale mwenye shabaha
aliyesilimu baada ya mapatano ya Hudaibia (Sulhul Hudaibiah), akawa Muislamu
mwema aliyepigana vita mbali mbali akiwa upande wa Waislamu, alishiriki katika
vita vya Al Yamamah chini ya uongozi wa Khalid bin Waliyd (Radhiya Llaahu
‘anhu) wakati majeshi ya Waislamu yalipopambana na majeshi ya Musailimah al
Kadhaab (Mtume wa uongo), na yeye ndiye mkubwa wa watoto wa Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) na alifariki dunia ghafla mahali panapoitwa Hibsh karibu na mji
wa Makka katika mwaka wa 53 H.
No comments:
Post a Comment